John 11

Kifo Cha Lazaro

1 aBasi mtu mmoja jina lake Lazaro alikuwa mgonjwa. Yeye alikuwa akiishi Bethania kijiji cha Maria na Martha dada zake. 2 bHuyu Maria, ambaye Lazaro kaka yake alikuwa mgonjwa, ndiye yule ambaye alimpaka Bwana mafuta na kuifuta miguu yake kwa nywele zake. 3 cHivyo hawa dada wawili walituma ujumbe kwa Isa kumwambia, “Bwana, yule umpendaye ni mgonjwa.”

4 dLakini Isa aliposikia hayo, akasema, “Ugonjwa huu hautaleta mauti bali umetokea ili kudhihirisha utukufu wa Mungu, ili Mwana wa Mungu apate kutukuzwa kutokana na ugonjwa huu.” 5Pamoja na hivyo, ingawa Isa aliwapenda Martha, Maria na Lazaro ndugu yao, 6 ebaada ya kusikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, aliendelea kukawia huko alikokuwa kwa siku mbili zaidi.

7 fNdipo akawaambia wanafunzi wake, “Haya, turudi Uyahudi.”

8 gWanafunzi wake wakamwambia, “Rabi, Wayahudi walikuwa wanataka kukupiga mawe, nawe unataka kurudi huko?”

9 hIsa akawajibu, “Si kuna saa kumi na mbili za mchana katika siku moja? Wala watembeao mchana hawawezi kujikwaa kwa maana wanaona nuru ya ulimwengu huu. 10 iLakini wale watembeao usiku hujikwaa kwa sababu hakuna nuru ndani yao.”

11 jBaada ya kusema haya, Isa akawaambia, “Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini naenda kumwamsha.”

12Wanafunzi wakamwambia, “Bwana, kama amelala usingizi ataamka.” 13 kHata hivyo, Isa alikuwa anazungumzia kuwa Lazaro amekufa, lakini wanafunzi wake hawakuelewa, walidhani kwamba anasema Lazaro amelala usingizi tu.

14Kwa hiyo Isa akawaambia waziwazi, “Lazaro amekufa. 15Hata hivyo nafurahi kwa kuwa sikuwepo huko kabla ya Lazaro kufa, ili mpate kuamini. Lakini sasa twendeni kwake.”

16 lTomaso aliyeitwa Pacha akawaambia wanafunzi wenzake, “Sisi nasi twendeni tukafe pamoja naye.”

Isa Ndiye Ufufuo Na Uzima

17 mIsa alipowasili huko alikuta Lazaro amekuwa kaburini siku nne. 18 nBasi Bethania ulikuwa karibu na Yerusalemu umbali wa karibu maili mbili,
Maili mbili ni kama kilomita tatu.
19 pWayahudi wengi walikuwa wamekuja kuwafariji Martha na Maria kwa ajili ya kufiwa na ndugu yao. 20 qMartha aliposikia kwamba Isa anakuja, alitoka kwenda kumlaki, ila Maria alibaki nyumbani.

21 rMartha akamwambia Isa, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa. 22 sLakini sasa ninajua kuwa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa.”

23Isa akamwambia, “Ndugu yako atafufuka.”

24 tMartha akamjibu, “Ninajua ya kuwa atafufuka wakati wa ufufuo wa wafu siku ya mwisho.”

25 uIsa akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo na uzima. Yeye aniaminiye mimi, hata akifa atakuwa anaishi 26 vna yeyote aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je, unasadiki haya?”

27 wMartha akamwambia, “Ndiyo Bwana, ninaamini ya kuwa wewe ndiwe Al-Masihi,
Al-Masihi maana yake ni Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.
Mwana wa Mungu, yeye ajaye ulimwenguni.”

Isa Alia

28 yBaada ya kusema haya Martha alikwenda, akamwita Maria dada yake faraghani na kumwambia, “Mwalimu yuko hapa anakuita.” 29Maria aliposikia hivyo, akaondoka upesi akaenda mpaka alipokuwa Isa. 30 zIsa alikuwa hajaingia kijijini, bali alikuwa bado yuko mahali pale alipokutana na Martha. 31 aaWale Wayahudi waliokuwa pamoja na Maria nyumbani wakimfariji walipoona ameondoka haraka na kutoka nje, walimfuata wakidhani ya kwamba alikuwa anakwenda kule kaburini kulilia huko.

32 abMaria alipofika mahali pale Isa alipokuwa, alipiga magoti miguuni Pake na kusema, “Bwana, kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa.”

33 acIsa alipomwona Maria akilia na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye pia wakilia, Isa alisikia uchungu moyoni, akafadhaika sana. 34Akauliza, “Mmemweka wapi?”

Wakamwambia, “Bwana, njoo upaone.”

35 adIsa akalia machozi.

36 aeNdipo Wayahudi wakasema, “Tazama jinsi alivyompenda Lazaro!”

37 afLakini wengine wakasema, “Je, yule aliyefungua macho ya kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”

Isa Amfufua Lazaro

38 agIsa kwa mara nyingine akiwa amefadhaika sana, akafika penye kaburi. Hilo kaburi lilikuwa pango ambalo jiwe lilikuwa limewekwa kwenye ingilio lake. 39 ahIsa akasema, “Liondoeni hilo jiwe.”

Martha ndugu yake yule aliyekuwa amekufa akasema, “Lakini Bwana, wakati huu atakuwa ananuka kwani amekwisha kuwa kaburini siku nne.”

40 aiIsa akamwambia, “Sikukuambia kwamba kama ukiamini utauona utukufu wa Mungu?”

41 ajKwa hiyo wakaliondoa lile jiwe kutoka kaburini. Isa akainua macho yake juu akasema, “Baba, ninakushukuru kwa kuwa wanisikia. 42 akNinajua ya kuwa wewe hunisikia siku zote, lakini nimesema haya kwa ajili ya umati huu uliosimama hapa, ili wapate kuamini ya kuwa wewe umenituma.”

43 alBaada ya kusema haya, Isa akapaza sauti yake akaita, “Lazaro, njoo huku!” 44 amYule aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono yake na miguu yake ikiwa imeviringishiwa vitambaa vya kitani na leso usoni pake.

Isa akawaambia, “Mfungueni, mwacheni aende zake.”

Shauri La Kumuua Isa

(Mathayo 26:1-5; Marko 14:1-2; Luka 22:1-2)

45 anHivyo Wayahudi wengi waliokuwa wamekuja kumfariji Maria, walipoona yale Isa aliyoyatenda wakamwamini. 46Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwaambia mambo Isa aliyoyafanya. 47 aoKwa hiyo viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaita mkutano wa baraza.

Wakaulizana, “Tufanyeje? Huyu mtu anafanya ishara nyingi.
48Kama tukimwacha aendelee hivi, kila mtu atamwamini, nao Warumi watakuja na kupaharibu mahali petu patakatifu na taifa letu.”

49 apMmoja wao aliyeitwa Kayafa, ambaye alikuwa kuhani mkuu mwaka huo, akasema, “Ninyi hamjui kitu chochote! 50 aqHamjui kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa lote liangamie?”

51 arHakusema haya kutokana na mawazo yake mwenyewe bali kama kuhani mkuu mwaka huo, alitabiri kuwa Isa angelikufa kwa ajili ya taifa la Wayahudi, 52 aswala si kwa ajili ya taifa hilo pekee, bali pia kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika, ili kuwaleta pamoja na kuwafanya wawe wamoja. 53 atHivyo tangu siku hiyo wakawa wanafanya mipango ili wamuue Isa.

54 auKwa hiyo Isa akawa hatembei hadharani miongoni mwa Wayahudi, bali alijitenga akaenda sehemu iliyo karibu na jangwa kwenye kijiji kiitwacho Efraimu. Akakaa huko na wanafunzi wake.

55 avBasi Pasaka ya Wayahudi ilipokuwa imekaribia, watu wengi walitoka vijijini wakaenda Yerusalemu kabla ya Pasaka ili wakajitakase. 56 awWatu wakawa wanamtafuta Isa, nao waliposimama kwenye eneo la Hekalu waliulizana, Je, mtu huyu hatakuja kamwe kwenye Sikukuu? 57Viongozi wa makuhani na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kuwa yeyote atakayejua mahali Isa aliko, lazima atoe taarifa ili wapate kumkamata.
Copyright information for SwhKC